Wanaume kama ilivyo kwa wanawake, na sisi tuna saikolojia yetu ya maisha. Usipotuelewa unaweza ukatuchukia wanaume wote duniani kwa sababu ya mwanaume mmoja au wawili uliowahi kuwa nao kwenye mahusiano.
Niseme tu jambo moja kwamba wanaume ni watu wazuri sana (japokuwa hakuna mkamilifu), lakini unapaswa kuwaelewa angalau kwa uchache ili kwenda nao sawa.
Katika mahusiano wapo wanaume wanaomaanisha kuwa na wewe hadi ndoa na pia wapo wababaishaji tu.
Ladies leo nataka kukuonesha aina 5 za wanaume ambao unapaswa kuwaepuka endapo una lengo la kuwa na mahusiano bora ya furaha…
1. Wanaume wapenda ngono.
Wapo wanaume wanaoamini kwamba hakuna upendo wa kweli bila kufanya mapenzi. Hili ni kundi ambalo kwa mantiki ya haraka hawana lengo la ndoa bali wanalenga kutimiza tamaa za mwili. Japokuwa wapo wanaojihusisha na ngono kabla ya ndoa na kufanikiwa kuoana, hilo halitakiwi kusifiwa au kupendekezwa kwa namna au sababu yoyote ile na jamii yetu.
Wanaume wapenda ngono wana mbinu kali za ushawishi, huanza taratibu kwa mambo madogo madogo, huonesha uaminifu mwanzoni lakini kwa namna ya masihara hujikuta wamekuangusha kwenye uzinzi. Watu wa namna hii wanajua kujali, hawajui kuonya ukikosea, ni wepesi kuitikia hitaji lako, anaweza kuahirisha kazi ili tu achati na wewe anapogundua u mpweke. Wana kila mbinu za kukupeleka dhambini. Ukithubutu kumpa penzi basi yote aliyokuwa anafanya mwanzoni yanapungua na baadaye kuisha na kukuacha kabisa. Usipompa penzi utakuja kugundua (ukiwa mdadisi) kwamba ana michepuko au baada ya muda atatafuta sababu za kuvunja mahusiano.
2. Wanaume “watoto”
Wanaume ambao wanaanza mahusiano lakini wana akili za kitoto. Si ajabu kumkuta mwanaume ambaye hawezi kufanya maamuzi bila mchango wa wazazi wake. Ukiwa na mwanaume kama huyo ujue dakika yoyote atakapoambiwa we humfai utaachika bila sababu. Wanaume wa aina hii mara nyingi wanapenda mambo ya kijinga, hawana muda wa kuwaza juu ya future yenu, hawako tayari kupoteza gharama au muda kwenye mambo muhimu isipokuwa kwenye starehe tu. Kifupi hawapendi kuzungumzia ndoa. Kuna tofauti kati ya wanaochelewa kuoa na wasiopenda ndoa, hapa nazungumzia wasiopenda kujadili kuhusu ndoa. Hukwepa kwa sababu kisaikolojia wao bado ni watoto.
3. Wanaume “wapenda ukamilifu”
Lugha nzuri tunaweza kuwaita “perfectionists” na sio vibaya ukawajumuisha na “judgementalists” kwenye kundi hili. Hawa ni wanaume ambao wanataka kila kitu kiende sawa sawa na kilivyopangwa.
Judgementalists ni wanaume wanaopenda kujudge kila kitu, yaani hakuna kitu utafanya wasiulize maswali. Hawajui kutia moyo, kusifia au kupongeza. Kuishi na wanaume wa namna hii ni lazima ujipange. Ni wepesi kubadili maamuzi bila kujali muda na rasilimali mlizotumia kwenye mahusiano yenu. Hawajali hisia za mtu mwingine, wanatumia “logic” zaidi, na kwa kweli ni wabinafsi kwa asili.
Kwa wanaojua saikolojia ya ndoa ambayo huhitaji maelewano, kujaliana, kusikilizana, kuvumiliana na kuchukuliana watakubaliana nami kwamba kundi hili la wanaume ni mzigo katika mahusiano. Mara nyingi wanaume wa namna hii huoa wanawake wadogo sana ili wawatawale kisaikolojia na kuwafanya watumwa.
4. Wanaume wenye mtazamo hasi (Negative minded men).
Japokuwa tabia hii ni mbaya kwa wote yaani wanaume na wanawake lakini inaweza kuleta athari kubwa kwa wanaume kwa sababu si wanaume wengi walio tayari kubadilika kitabia. Mara nyingi wanaume wanapenda wanawake wabadili tabia ili kuwafaa wanaume na sio kinyume chake. Sababu za kuwa na mtazamo hasi ni nyingi kutokana na mtu mmoja na mwingine. Wengine ni kwa sababu ya kutojiamini, wengine ni kutokana na mambo ambayo umewahi kumfanyia kwenye mahusiano yenu, wengine historia za maisha yao ya utotoni na wengine ni kwa sababu ya wivu uliopitiliza kwa hiyo anawaza kuibiwa tu na mengine mengi.
Kwa nini watu hawa sio potential kwa wanawake? Ni kwa sababu wanawake wanapenda mwanaume anayejali, anayepongeza na kusifia, mwenye mtazamo wa kutoshindwa, lazima mwanaume ujue kwamba mwanamke hujihisi hayuko salama (insecured) endapo kila anachofanya unaonesha kukitazama kwa ubaya. Badili mtazamo wako utaanza kuona uzuri wa mwenzio kwenye mahusiano.
5. Wanaume wanaoigiza maisha (pretenders)
Hawa ni wanaume ambao hawajakubali hali zao za maisha. Kama ni maskini atataka aonekane tajiri. Akijuana na mtu maarufu basi na yeye anataka aonekane maarufu. Wanaume wa namna hii ukiwagundua hawaoni shida kuvunja mahusiano ili kuficha aibu yao. Wanataka kufanana na wanaume watoto. Kifupi hawa ni wanaume ambao hawana mikakati thabiti ya maisha yao, hufuata upepo na mara nyingi hawana uwezo wa kweli wa kutunza familia. Ili kuolewa na mwanaume wa jinsi hii mwanamke anapaswa kumfahamu kabla ili ajue hatua muhimu za kumbadilisha.
No comments:
Post a Comment