SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara yake ya Vijana Sanaa Utamaduni na Michezo leo imetoa taarifa na ufafanuzi juu ya timu yake ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 (Karume Boys) ambayo imeondolewa kwenye Mashindano ya CECAFA U-17 yanayoendelea nchini Burundi.
Katibu mkuu wa Wizara hiyo Omar Hassan (King) ametoa ufafanuzi huo mbele ya Waandishi wa Habari kuhusu kadhia hiyo iliyotea kwa Vijana wa Zanzibar huko nchini Burundi ambapo amesema ikithibitika kuwa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) wao ndio wenye makosa mpaka Karume Boys wakaondoshwa katika Mashindano basi wajiwajibishe wenyewe kwa kujiuzulu.
"Kama itakuwa kosa lao ZFA na kama Mimi nimo ZFA basi ntakaa pembeni, naamini na wao wenyewe watatumia busara ya hali ya juu kukaa pembeni".
Zanzibar iliondolewa katika Mashindano hayo na kupigwa faini kwa kosa la kuorodhesha wachezaji waliozaliwa kabla ya 01/01/2002 ambapo kanuni ya Mashindano hayo iliwataka wachezaji waliozaliwa kuanzia 01/01/2002 huku Zanzibar ikuwapeleka wachezaji 12 waliozaliwa 2001 jambo ambalo ZFA wamesema hawana taarifa kama wachezaji walotakiwa waliozaliwa 2002 ambapo wao walijuwa walokuwa na umri chini ya miaka 17 hivyo hata walozaliwa 2001 ikiwa bado hawajafika miaka 17 walifikiri wanaruhusiwa ndio mana wakaenda nao ambapo katibu Mkuu wa CECAFA Nicholaus Musonye alisema kuwa ZFA walitumiwa ufafanuzi wa umri kwenye Barua Pepe labda hawazisomi tu.
Kutokana na makosa hayo Karume boys imepewa adahabu tatu ikiwemo kuondolewa mashindanoni, inaambatana na faini dola 15,000 (Sh 30 milioni) zinazotakiwa kulipwa na Chama cha Soka la Zanzibar (ZFA), ambapo fedha hizo zitafidia gharama za tiketi, malazi na chakula ya timu katika kipindi chote walichokaa Burundi huku adhabu ya tatu ikiwa kufungiwa kutoshiriki mashindano yanayoendeshwa na CECAFA hadi hapo watakapolipa faini hiyo ambayo inatakiwa kurudishwa FIFA.
Karume boys ilikuwa icheze juzi Jumapili mchezo wake wa kwanza dhidi ya Sudan katika uwanja wa Gitega mchezo ambao haukuchezwa baada ya Sudan kupeleka malalamiko yao kwa CECAFA na mchezo huo ukafutwa ambapo Vijana hao wanategemea kurejea nyumbani leo majira ya saa 2 za usiku.
No comments:
Post a Comment