MABINGWA watetezi, Azam FC wamefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati baada ya ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Pongezi kwake shujaa wa timu hiyo leo, mshambuliaji chipukizi, Shaaban Iddi Chilunda aliyefunga mabao yote manne peke yake katika dakika za 19, 33, 39 na 64 katika michuano yake ya kwanza ya Kombe la Kagame.
Ikumbukwe Chilunda anacheza kwa mara ya mwisho Azam FC kabla ya kwenda Hispania kuanza kuutumikia mkataba wa mkopo wa miaka miwili Tenerife ya Daraja la Pili Hispania.
Mabao ya Rayon Sports inayoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa Kundi D pamoja na vigogo wa Tanzania, Yanga SC yamefungwa na Rwatubyaye Abdul dakika ya 42 na Manishimwe Djabel dakika ya 81.
Azam FC sasa inatangulia Nusu Fainali na itakutana na mshindi wa Nusu Fainali ya pili, kati ya Singida United na JKU ya Zanzibar.
Tayari Simba na Gor Mahia zimetangulia katika hatua ya Nusu Fainali ya michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu, kufuatia jana kuzitoa Vipers ya Uganda na AS Ports ya Djibouti.
Ilianza Gor Mahia kutoka nyuma na kushinda 2-1, baada ya kutanguliwa na Vipers kwa bao la Thadeo Lwanga dakika ya 17, kabla ya kuzinduka na kusawazisha kwa mabao ya Francis Mustafa dakika ya 48 na 75.
Mchezo wa pili, Mohamed Rashid akatokea benchi dakika ya 59 kwenda kuchukua nafasi ya Adam Salamba na kuifungia Simba bao pekee dakika ya 65 dhidi ya AS Ports.
No comments:
Post a Comment