SIMBA YAITWANGA YANGA KARIAKOO DERBY - ALEX MWENDATZ

Breaking

Sunday, April 29, 2018

SIMBA YAITWANGA YANGA KARIAKOO DERBY


BAO pekee la beki Erasto Edward Nyoni limetosha kuipa ushindi wa 1-0 Simba SC dhidi ya mahasimu wao, Yanga SC jioni ya leo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ni ushindi ambao unawasogeza kabisa Wekundu hao wa Msimbazi kabisa na taji la kwanza la ubingwa wa Ligi Kuu tangu mwaka 2012, kwani sasa inafikisha pointi 62 baada ya kucheza mechi 26 na sasa itahitaji kushinda mechi mbili ili kujihakikishia ubingwa, lakini shughuli inaweza kuwa nyepesi kama Yanga yenye pointi 48 za mechji 24 sasa itapoteza tena mechi  zake mbili zijazo.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Emmanuel Mwandembwa wa Arusha aliyesaidiwa na Frank Komba wa Dar es Salaam na Mohammed Mkono wa Tanga, Nyoni alifunga bao lake hilo dakika ya 37 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na winga Shiza Ramadhani Kichuya.


Dalili za Simba kupata bao zilionekana mapema tu, kutokana kuutawala mchezo dhidi ya wapinzani wao ambao hawakuwa na makali kabisa katika safu yao ya ushambuliaji.
Sifa ziwaendee walinzi wa Yanga, wakiongoza na mkongwe, Kelvin Patrick Yondan kwa kuwadhibiti vizuri washambuliaji hatari na wenye uchu wa Simba, akina Kichuya, Mganda Emmanuel Okwi na Nahodha, John Raphael Bocco.
Kipindi cha pili Yanga ilikianza vibaya baada ya kupata pigo kufuatia beki wake wa kulia, Hassan Ramadhani Kessy kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 48 kwa kumchezea rafu beki Mghana, Asante Kwasi.  
 
Na hapo ndipo matumaini ya ushindi kwa mabingwa hao watetezi yalipozima na kuanza kucheza kwa tahadhari kujizuia kuruhusu mabao zaidi ya wapinzani wao.
Simba SC ilistahili ushindi wao leo kutokana na mchezo mzuri na ubora wa kikosi chake ni bahati tu iliyowakosesha mabao zaidi.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Nicholas Gyan/Paul Bukaba dk83, Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Yussuf Mlipili, James Kotei, Jonas Mkude, Shomary Kapombe, John Bocco, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya.
Yanga SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Andrew Vincent 'Dante', Kelvin Yondan, Said Juma 'Makapu', Yussuf Mhilu, Papy Kabamba Tshishimbi/Emmanuel Martin dk80, Obrey Chirwa, Raphael Daudi/Juma Mahadhi dk46 na Ibrahim Ajib/Pius Buswita dk62.

No comments:

Post a Comment