Rekodi za Okwi CAF yawasumbua Yanga. - ALEX MWENDATZ

Breaking

Wednesday, April 11, 2018

Rekodi za Okwi CAF yawasumbua Yanga.


ACHANA kabisa na Emmanuel Okwi, huyu jamaa si mtu mzuri kabisa. Takwimu za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zimefichua kuwa, straika huyo wa Simba ana rekodi ambayo si tu imewashinda mastraika nchini, bali Afrika nzima.


Licha ya kuwa Simba tayari imeondoshwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Okwi ameacha rekodi ya kupachika mabao Afrika.

Kama ulikuwa hufahamu, Okwi ndiye staa pekee aliyefunga katika mechi tatu mfululizo za Shirikisho, hivyo kuwatega mastaa wa Yanga ambao wanahitaji sare tu ugenini ili kufuzu hatua ya makundi.

Okwi, ambaye anashika nafasi ya pili kwa kupachika mabao kwenye michuano hiyo, alifunga kwenye mechi mbili dhidi ya Gendarmerie ya Djibouti kisha kufunga tena dhidi ya Al Masry kwenye mechi iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Mchezaji mwingine aliyeweza kufunga mabao kwenye mechi tatu mfululizo ni Felix Badenhorst wa Mbabane Swallows ya Swaziland, lakini amefanya hivyo kwenye michuano Ligi ya Mabingwa.

Mpaka sasa hakuna mchezaji yeyote wa Yanga aliyefunga mabao mawili kwenye mashindano ya kimataifa. Nyota wa Yanga, Juma Mahadhi, Emmanuel Martins, Ibrahim Ajibu na Raphael Daudi kila mmoja amefunga mara moja kwenye mashindano hayo.

MSUVA HUYOO

Staa wa Tanzania, Saimon Msuva anahitaji mabao matatu ama zaidi ili kuibuka mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Msuva anashika nafasi ya pili akiwa amefunga mara nne, na kuzidiwa mawili tu na Hamid Ahaddad pia wa Difaa El Jadida.

Jadida ya Msuva tayari ipo hatua ya makundi ya michuano hiyo ikiwa imepangwa na timu za TP Mazembe, MC Alger na Es Setif za Algeria.

No comments:

Post a Comment