Safari ni hatua, baada ya kuanza utafutaji wa maisha yake ya soka kwa kujiunga na Akademi ya Aspire miaka michache iliyopita, hatimaye winga, Nasry Aziz yuko mbioni kuhitimu.
Miaka imekatika na hatimaye umefika muda kwa kinda huyo wa Kitanzania kujiandaa na maisha mengine nje ya Akademi iliyomkuza kwa kumfundisha misingi ya soka nchini Senegal.
Mradi wa Aspire nchini ulianza mchakato wa kusaka vijana mwezi Machi-Mei, 2014 ambapo vijana wengi walijitokeza na kuchaguliwa vijana 14 ambao walikwenda katika mchujo mwingine uliofanyika nchini Uganda uliowashirikisha vijana zaidi ya 50.
Kijana huyo ni miongoni mwa wachezaji 17 waliochaguliwa kati ya vijana 34 waliokuwepo nchini Senegal kwa muda wa mwezi mmoja, ambapo kulikuwa na vijana wengi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na Amerika ya Kusini.
Kituo cha Aspire kilichopo Dakar nchini Senegal ni miongoni mwa vituo viwili vinavyoongozwa na mtoto wa mfalme wa Qatar, Hamad bin Khalifa Al Thani huku kingine kikiwa mjini Doha.
Hamad ana uhusiano wa karibu na Barcelona ya Hispania kutokana na uwekezaji ambao wameufanya kwenye klabu hiyo, uhusiano huo umevifanya vituo vyake kuwa na maelewano mazuri na kituo cha Barcelona, La masia.
Spoti Mikiki imezungumza na Nasry kwa marefu na mapana akiwa mjini, Dakar ambaye amezungumzia mipango iliyopo mara baada ya mkataba wake kumalizika mwezi, Juni mwakani kuwa atapambana kuhakikisha anatoka kisoka.
“Siku zimesogea kabisa, umefika muda wa kujiandaa na maisha kamili ya soka na sio ya darasani tena, nimejifunza mengi ambayo naamini yatakuwa msingi kwangu kwenye uchezaji wangu.
“Uwezekano wa kupata timu za kuzichezea ni mkubwa kwa sababu kama kuonyesha kuvutiwa na uwezo wangu wapo ambao wameonesha kunihitaji kwa kusubiri mkataba wangu utakapo malizika.
“Nimekuwa nikiongea na kaka yangu kwenye hii kazi ya mpira, Orgeness Mollel ambaye yupo Ureno kwenye klabu ya Famalicao, amekuwa akinihamasisha kwa kuwa naye amepitia kwenye hiki kituo pia amenionyesha njia za kupita, “ anasema Nasry.
Anaendelea : “Nina watu ambao wananisimamia lakini pia kwa upande wangu nimejijengea tabia ya kuwa, naongea na watu ambao wamenitangulia ili kupata mwanga wa kuona mbele kulivyo. “
Katika mafunzo hayo ambayo wamekuwa wakiyapata kwenye kituo hicho kilichopo, Dakar, Nasry anasema wamekuwa wakiyafanyia kazi kwenye mashindano mbalimbali ya vijana ambayo pia yanahusisha, timu ya Akademi ya La Masia.
“Kila msimu huwa tunakwenda kwenye mashindano ya vijana, lakini kwa msimu huu hatujaenda, Hispania ambako tulikuwa na nafasi ya kwenda kuonyesha vipaji vyetu.
“Mawakala mbalimbali wanatembelea mashindano yetu na kutengeneza ukaribu na wasimamizi wa wachezaji pamoja na vituo ambavyo wachezaji wanatoka,” anasema Nasry.
Hata hivyo, kinda huyo anasema ndoto yake ni kucheza soka la kulipwa barani Ulaya kama ilivyo kwa wenzake, Mollel ambaye anacheza Ligi Daraja la Kwanza, Ureno na Martin Tangazi ambaye yupo, GaziÅŸehir Gaziantep F.K. ya Uturuki.
“Wote hao wamepitia kwenye hiki kituo na taarifa zao ninazo kuwa walifanya vizuri na ndiyo maana muda wao ulipofika wa kuondoka kwenye kituo hawakupata shida kabisa kwenye kutafuta timu za kujiunga nazo.
“Tangazi alifanya vizuri sana dhidi ya Barcelona ya vijana mechi zilikuwa kule Qatar baada ya mashindano yale na mkataba wake na kituo kumalizika, alichukukiwa na GaziÅŸehir ambao inasemekana walikuwa wakimfuatilia kwa zaidi ya miezi sita.
“Natakiwa kuendelea kucheza kwenye kiwango cha juu katika mechi zetu mbalimbali ambazo huwa tunacheza za kirafiki mbali na mashindano ili niendelee kuwa kwenye mazingira mazuri ya kupata timu kubwa,” anasema.
Kuhusu ratiba yake ya mazoezi binafsi, Nasry anasema kuwa amekuwa akitumia muda wake wa ziada kwenye kukimbia sehemu zenye fukwe ili kuwa fiti zaidi akiwa uwanjani.
Nasry hakusita kuongelea uwezekano wa kuzichezea timu za taifa za vijana kwa kusema bado anatamani kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoitwa ambao watalitumikia taifa kwenye ngazi hiyo.
“Kuitwa au kutoitwa timu ya taifa ni uamuzi wa kocha lakini nitafurahi siku akiniita, wapo wenzetu hapa wanaitwa na timu zao za vijana na wakimaliza wanarudi hapa,” anasema kinda huyo ambaye mwaka huu atatimiza miaka 17.
Pamoja na yote Nasry anasema kila kitu kitakuwa sawa na itafika hatua ya kuitwa na kulitumikia taifa sio lazima kwenye ngazi ya vijana hata kwenye kikosi cha wakubwa,Taifa Stars.
Nyota huyo aliwahi kuonjeshwa jezi ya Taifa Stars kwa kupata nafasi ya kufanya nao mazoezi mwishoni mwa mwaka jana mara baada ya kurejea nchini kwa mapumziko mafupi akitokea, Dakar.
No comments:
Post a Comment