POINTI 52 Kibindoni. Naam, Wekundu wa Msimbazi, Simba SC leo wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuwachapa wenyeji, Mtibwa Sugar 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Ni ushindi ambao unaifanya Simba SC ifikishe pointi 52 katika mechi ya 22 ikiendeleza kuongoza Ligi Kuu kwa pointi sita zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 46 za mechi 21, wakati Mtibwa Sugar inabaki katika nafasi ya sita na pointi zake 30 za mechi 22 pia.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abubakar Mturo wa Mtwara aliyesaidiwa na Omary Juma na Khalfan Sika wa Pwani, hadi mapumziko Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji Mganda, Emmanuel Arnold Okwi dakika ya 23 kwa shuti akiwa ndani ya boksi baada ya pasi ya kichwa ya Nahodha John Raphael Bocco aliyeunganisha krosi ya winga Shiza Ramadhani Kichuya.
Bao hilo liliwazindua Mtibwa Sugar ambao walikuwa wanacheza taratibu na kuanza kupeleka mashambulizi kwa kasi langoni mwa Simba SC kusaka bao la kusawazisha.
Lakini Mtibwa Sugar walio chini ya kocha Zuberi Katwila, mchezaji wake wa zamani iliishia kukosa mabao ya wazi kutokana na umakini mdogo kwenye kumalizia wa washambuliaji wake.
Simba SC ya kocha Mfaransa, Pierre Lechantre nayo haikupoa, kwani iliendelea kujibu mashambulizi hayo na dakika hya 40 almanusra Okwi afunge tena kama si shuti lake kuokolewa na kipa benedicto Tinocco.
Kipindi cha pili, timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu, lakini dakika 20 za mwisho Simba SC wakaanza kucheza kwa kujihami na Mtibwa Sugar wakaendelea kukosa mabao ya wazi.
Kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa; Benedictor Tinocco, Kibwana Ally Shomary, Hassan Mganga, Hassan Isihaka, Dickson Daudi, Shaabani Mussa Nditi, Salum Kihimbwa, Henry Joseph Shindika, Stahmil Mbonde/Hussein Javu dk63, Hassan Dilunga/Ayoub Semtawa dk73 na Ismail Aidan Mhesa/Haroun Chanongo dk65.
Simba SC; Aishi Manula, Nicholas Gyan/Haruna Niyonzima dk76, Asante Kwasi, Paul Bukaba, Yussuf Mlipili, Joanas Mkude, Shomary Kapombe, Muzamil Yassin/Salim Mbonde dk66, John Bocco, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya.
No comments:
Post a Comment