Na Alex Mwenda
Achana na Abdi Banda. Huyu umemzoea, bonge moja la beki tegemeo la Tanzania anayechezea Baroka FC ya Afrika Kusini.
Juzi tu aliokoa mabao mawili dhidi ya Rwanda hapo Uwanja wa Taifa.
Pia kuna hawa, kipa, Deogratius Munish ‘Dida’ wa University of Pretoria na Uhuru Suleiman anayechezea Mthatha Bucks zote za huko Bondeni.
Sasa sikia, kuna huyu mwingine anachezea Jomo Cosmos ya Afrika Kusini. Ni bonge moja la straika anaitwa Ismail Mohamed Mgunda.
Alikuwa mshambuliaji wa zamani wa Coastal Union ya Tanga, na alijiunga na Jomo Cosmos ya Afrika Kusini kwa kusaini mkataba wa miaka miwili, baada ya kufuzu majaribio ya wiki mbili.
Jomo Cosmos ni timu ya Daraja la Kwanza ambayo ipo kwenye nafasi nzuri ya kushiriki Ligi Kuu nchini humo kama itamaliza vizuri michezo yake minne iliyosalia kwenye ligi hiyo, kabla ya jana (Jumapili) kucheza na Royal Eagles.
Mgunda alijiunga na timu hiyo ambayo mara yake ya mwisho kushiriki Ligi Kuu Afrika Kusini ‘PSL’ ilikuwa msimu wa 2015/2016 akitokea Gilport Lions FC ya Botswana.
Spoti Mikiki imefanya mazungumzo ya kina na mshambuliaji huyo ili kujua ilikuwaje akapata nafasi ya kufanya majaribio, Jomo na mara baada ya kufuzu majaribio hayo,mchakato wa kujiunga na timu hiyo ulikuwaje.
“Kwanza kabisa kabla ya kwenda, Botswana kucheza mpira wa kulipwa nilianza kuichezea Coastal ya Tanga kwa msimu mmoja wa 2015/2016, msimu uliofuata nikajiunga na Ruvu Shooting, baada ya kuichezea Ruvu msimu mmoja ndiyo nikaenda zangu Botswana.
“Tangu naanza kucheza mpira hata kabla ya Samatta kwenda Ulaya, nilikuwa na ndoto ya kuwa mchezaji wa kulipwa, ndiyo maana hata ukiangalia hakuna timu ya ndani ambayo nimeichezea kwa zaidi ya msimu mmoja.
“Kila nilipokuwa napita nilikuwa napatumia kwa sehemu ya kujijengea CV ili nikiomba nafasi sehemu kufanya majaribio nisikutane na ugumu,” anasema Mgunda.
Wakati anatua Botswana na kusaini mkataba wa miaka miwili,Mgunda alikuwa tayari ameshatuma CV zake za kuomba kujiunga na Jomo ambao walijipa muda kabla ya kuamua kumuita kwa majaribio.
“Nilienda Botswana kwa sababu matumaini yangu ya kwenda, Afrika Kusini yalikuwa yamefifia kutokana na kutojibiwa majibu yangu kwa wakati niliokuwa nimetarajia.
“Tulianza vizuri msimu lakini Gilport Lions FC haikuwa timu kubwa, tulikutana na wakati mgumu mbele ya vigogo wa nchini hiyo kama Township Rollers, Galaxy, Orapa United, Gaborone United, Miscellaneous na BDF XI.
“Huwezi kuamini kwenye kipindi cha zaidi ya nusu msimu tuliambulia kushinda mchezo mmoja pekee na kufungwa zaidi ya mara 10 huku sare zikiwa tano,sisi ndiyo tuliokuwa wa mwisho kwenye msimamo wa ligi,” anasema.
Anaendelea; “Nikiwa kwenye mazingira hayo magumu kwa maana ya timu kushindwa kupata matokeo ndiyo nikapata majibu ya kuitwa na Jomo,Afrika Kusini kwaajili ya kwenda kufanya majaribio hayo ya wiki mbili.
“Uzuri mkataba niliokuwa nimesaini, Gilport Lions FC wa miaka miwili ulikuwa na kipengele cha kuondoka muda wowote endapo nikipata timu ya kuichezea sehemu nyingine.
Mgunda anasema baada ya kupata mualiuko huo wa kwenda Afrika Kusini aliongea vizuri na viongozi wake wa Gilport ambao nao walibariki safari hiyo na kumweleza kama atashindwa milango ipo wazi ya kurejea.
“Suala la kushindwa huwa silipendi kwenye uchezaji wangu soka, niliona ni kama tayari mlango wa neema umefunguka na kilichosalia ni kwenda kuonyesha uwezo wangu ili wanipe nafasi ya kujiunga nao.
“Nilipokelewa vizuri, Johannesburg na mara moja nikaanza maharibio ya wiki hizo mbili kwa kujumuika na kikosi cha kwanza kwenye mazoezi, nilijua labla nitapimwa kwa kucheza mchezo wa kirafiki ili wahakiki uwezo wangu.
“Lakini ilikuwa tofauti kwa sababu kocha wa timu hiyo, Jomo Sono na benchi lake la ufundi, lilivutiwa na uwezo wangu kwenye mazoezi tu ya wiki mbili ambayo niliyafanya na timu yao na kuamua kunipa mkataba,” anasema.
Mbali ya kuwa Jomo Sono ni kocha wa Jomo Cosmos pia ni mmiliki wa timu hiyo ambayo ipo nafasi ya tatu na pointi 42, wamezidiwa pointi 17 na vinara wa ligi hiyo, Highlands Park wenye pointi 59, kabla ya michezo ya jana.
Hata kama Jomo watamaliza nafasi ya tatu watakuwa kwenye nafasi ya kucheza mchujo wa kuwania nafasi ya kupanda daraja.
No comments:
Post a Comment