YANGA SC KUONDOKA JUMAPILI ASUBUHI KUFUATA TIKETI YA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA ETHIOPIA - ALEX MWENDATZ

Breaking

Saturday, April 14, 2018

YANGA SC KUONDOKA JUMAPILI ASUBUHI KUFUATA TIKETI YA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA ETHIOPIA

MABINGWA wa Tanzania, Yanga SC wataondoka Jumapili asubuhi kwenda Hawassa, Ethiopia tayari kwa mchezo wao wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika katikati ya wiki ijayo dhidi ya wenyeji, Wolaita Dicha.
Yanga watakuwa wageni wa Wolaita Dicha Jumatano jioni Uwanja wa Hawassa mjini Hawassa wakitoka kushinda 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
Lakini kuelekea mchezo huo wa marudiano ambao Yanga wanatakiwa kwenda kuulinda ushindi wao kwenye mchezo wa kwanza, hawatakuwa na kocha wao Mkuu, Mzambia, George Lwandamina aliyeondoka mapema Jumanne kwenda kukamilisha mipango ya kurejea Zesco United ya kwao.

Image result for yangaZesco United imeamua kumrejesha kocha wake huyo baada ya mafanikio yake Tanzania ndani ya miaka miwili, akiiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita na sasa inakaeribia kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Lwandamina alijiunga na Yanga Novemba mwaka 2016 akichukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm na katika kipindi hicho ameiongoza timu katika michezo 77 ya mashindano yote akitoa sare 18, kushinda 45 kati ya hizo mbili kwa penalti baada ya sare ndani ya muda wa kawaida na kufungwa 14, tano kwa penalti baada ya sare katika muda wa kawaida.
Kwa sasa benchi la Ufundi la Yanga lipo chini ya walimu watatu waliokuwa Wasaidizi wa Lwandamila, Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazawa, Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali.

No comments:

Post a Comment