MSHAMBULIAJI wa Maji Maji ya Songea, Jerson ‘Jerry’ John Tegete amesema kwama watapigana hadi tone la mwisho la damu kuhakikisha wanainusuru timu hiyo kushuka Daraja Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Maji Maji jana imechapwa 3-2 na wenyeji, Mwadui FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.
Maji Maji jana imechapwa 3-2 na wenyeji, Mwadui FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.
Matokeo hayo yanaifanya timu hiyo ya Ruvuma iendelee kuburuza mkia katika Ligi Kuu ya timu 16, ikibaki na pointi zake 16 baada ya kucheza mechi 23, nyuma ya Njombe Mji FC yenye pointi 18 za mechi 22, Mbao FC yenye pointi 20 za mechi 23 na Kagera Sugar yenye pointi 21 za mechi 22 pia zikifuatana mkiani.
Katika mchezo wa jana, mabao ya Mwadui FC yalifungwa na Paul Nonga dakika ya sita na 56 na Miraj Athumani wakati ya Maji Maji yalifungwa na Marcel Boniventura Kaheza yote mawili, dakika za 64 na 85.
Lakini akizungumza na ALEX MWENDATZ leo, Tegete amesema kwamba matokeo ya jana ni mabaya kwao, lakini wataendelea kupambana hadi dakika ya mwisho na watatoa hadi tone lao la mwisho la damu kuhakikisha wanafanya vizuri.
“Hali ni mbaya kwa kweli, lakini sisi hatujakata tamaa, tutaendelea kupigana hadi dakika ya mwisho kuhakikisha tunainusuru timu isishuke,”amesema.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, amesema kwamba wana mechi mbili za nyumbani dhidi ya Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar ambazo watajitahidi washinde, lakini pia mechi zao mbili zijazo za ugenini dhidi ya Stand United mjini Shinyanga na baadaye Mbao FC mjini Mwanza watajitahidi washinde pia.
“Na kwa sababu tupo wengi pale chini na hatutofautiani sana kwa pointi na wenzetu wengine hawajacheza zile mechi lazima wafungwe na Azam, SImba na Yanga, kwa kweli bado tuna matumaini tukifanya vizuri kwenye mechi zilizobaki tunaweza kunusurika,”amesema mshambuliaji tegemeo wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars.
Kutakuwa na mchezo mmoja zaidi kesho, vinara wa ligi, Simba SC wakiwa wageni wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
No comments:
Post a Comment