Mkwela: Nilimchana mzungu lakini akabebwa - ALEX MWENDATZ

Breaking

Monday, April 2, 2018

Mkwela: Nilimchana mzungu lakini akabebwa



Bondia wa uzani wa light, Idd Mkwela ameanza kutajwa kama bondia ambaye anaweza kufika mbali kwenye mchezo huo wa masumbwi kutokana na uwezo wake wa kurusha makonde.
Hivi karibuni, Mkwela mwenye miaka 28,alipoteza pambano lake la kwanza nchini Latvia kwa pointi za majaji 2-1 dhidi ya mwenyeji wake Andrejs Podusovs.
Licha ya Mkwela kupoteza pambano hilo, alimtwanga makonde vilivyo Mlatvia huyo na kupasuka maeneo ya usoni lakini hata hivyo hakupewa ushindi wa TKO.
Sapoti Mikiki imefanya mazungumzo na bondia huyo ambaye amedai kupoteza kwa mchezo wake uliopita kumempa somo la namna ya kucheza, ugenini, lakini pia aligusia alivyoanza kujihusisha na masumbwi.
“Nilianza kucheza ngumi mwaka 2010 kwa mwalimu wangu ambae anaitwa, Dungu Stailys ndo akawa ananichukuwa ananipeleka kwa mwalimu wake ambae anaitwa, Iraq Udu, nyumbani kwake Buguruni tulikuwa tunatoka Magomeni mpaka Buguruni.
“Lakini yote hiyo ilichangiwa na tabia yangu ya kwenda mara kwa mara kwa Dungu ambaye alikuwa akiwafundisha vijana wake, alivyokuwa akiniona kila siku natazama mazoezi pale aliniita siku moja na kuniambia nijiunge naye huo ndo ukawa mwanzo wa kujiunga naye, “ anasema Mkwela.
Bondia huyo ambaye amecheza mapambano tisa na katika mapambano hayo ameshinda mara saba kwa KO, droo mara moja na kupoteza mara moja, amesema changamoto alizokutana nazo kwenye mchezo huo ni nyingi.
“Changamoto kubwa kwa bondia mchanga ni uwezo wa kujihudumia kwa sababu wakati unaingia kwenye ngumi lazima uanze kwa kujitolea,nimetembea sana kwa mguu kutoka Magomeani hadi Buruguni ambako nilikuwa nikifanya mazoezi,” anasema
Hata hivyo, Mkwela mwenye ndoto ya kuwa bondia mkubwa Afrika na Duniani kote anasema kilichomwangusha Latvia ni kutokuwa na hesabu nzuri za kumtwanga mpinzani wake kwa KO.
Bondia huyo mwenye futi tano ni wanne nchini kwenye orodha ya mabondia bora wa uzani wake kati ya mabondia 90.
Katika msururi huo wa viongozi, anayeongoza kwenye orodha hiyo ni Benson Nyilawila wakati anayefuatia ni Mohammed Kambuluta pamoja na Adam Ngange.

No comments:

Post a Comment