Serikali: Madola msiende kugeuka watalii Australia - ALEX MWENDATZ

Breaking

Thursday, March 29, 2018

Serikali: Madola msiende kugeuka watalii Australia

Serikali: Madola msiende kugeuka watalii Australia


Dar es Salaam. Serikali imewataka wanamichezo wanaokwenda kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola kurejea nchini na medali.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amewataka wachezaji wa timu ya Taifa kutogeuka wasindikizaji au watalii nchini humo.
Dk Mwakyembe alisema itakuwa aibu kwa wachezaji wa timu hiyo kwenda kuwasindikiza wengine katika michezo hiyo iliyopangwa kuanza Aprili 4 hadi 15, mwaka huu.
Michezo ya Madola inayochezwa kila baada ya miaka minne, inatarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Carrara katika mji wa Gold Coast, Australia.
Dk Mwakyembe alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana, katika hafla ya kuwakabidhi Bendera ya Taifa wachezaji wa timu hiyo yenye wachezaji 16.
“Msiende kutalii wala kusindikiza wengine, najua mmejiandaa vya kutosha katika maandalizi yenu mwende mkapambane. Miguu na mikono yenu ndiyo utajiri wenu hivyo mkaitumie kikamilifu Australia,” alisema Dk Mwakyembe.
Pia alisema kuwa kuondolewa baadhi ya wanariadha kwenye timu hiyo kusiwapunguzie morali ya kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Awali, Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Nchini, Alex Mkeyenge aliwataka wachezaji hao kuacha kutoa visingizio endapo watarejea mikono mitupu kwa madai kuwa wamepata maandalizi ya kutosha kabla ya kupaa kwenda Australia.
“Hatutaki kusikia visingizio kwamba hamkujiandaa mtakaporejea baada ya michezo, anayejiona hayuko fiti bora aseme asiende, lakini suala la visingizio hatutaki,” alisema.
Nahodha wa timu hiyo, Issa Mtalaso alisema wamejiandaa vyema na ametoa ahadi kwa Watanzania kuwa wanakwenda kushindana na watarejea na medali.
Timu ya riadha inaundwa na Said Makula, Failuna Abdi, Stephano Huche, Sarah Ramadhani, Ali Gullam na Anthony Mwanga.
Ngumi Kassim Mbutike, Selemani Kidunda, Ezra Paul na Haruna Swanga.
Waogeleaji, Hilal Hilal na Sonia Tumiotto. Wachezaji wa tenisi ya meza, Amoni Amani, Masoud Mtalaso, Neema Mwaisyula na Fathiya Pazi.
Makocha ni Zacharia Barie na Lwiza John (riadha), Benjamini Oyombi (ngumi), Ramadhani Othman (tenisi ya meza) na Khalid Lushaka (kuogelea).

No comments:

Post a Comment