Dawa kupata Stars bora hii hapa - ALEX MWENDATZ

Breaking

Thursday, March 29, 2018

Dawa kupata Stars bora hii hapa




Dar es Salaam. Mchezo wa kimataifa baina ya timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ dhidi ya DR Congo, umeonyesha Tanzania inahitaji idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa.
Kitendo cha kutegemea wachezaji wa ridhaa, kinaweza kuigharimu Tanzania katika kushiriki mashindano ya kimataifa hasa Afcon kwa baadaye.
Taifa Stars juzi ilivuna mabao 2-0 dhidi ya DR Congo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini ushindi huo ulichagizwa kwa kiasi kikubwa na wachezaji watatu wanaocheza soka la kulipwa.
Nahodha Mbwana Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji, Saimon Msuva (Difaa El Jadida ya Ligi Kuu ya Morocco na Abdi Banda wa Baroka ya Afrika Kusini, walionyesha tofauti ya kiufundi na wachezaji wa ndani. Mwingine ni Rashid Mandawa wa BDF ya Botswana.
Samatta, Msuva na Banda walicheza kwa nidhamu ya mchezo hatua na walichangia kuibadili timu katika idara zote.
Nahodha huyo alionyesha ni kiongozi uwanjani, kwa sababu mara kadhaa alikuwa akitoa maelekezo kwa wachezaji wenzake timu ilipokuwa na mpira au ikishambuliwa.
Samata, Msuva na Banda kwa nyakati tofauti walionekana wakitoa maelekezo hatua inayoonyesha kuwa kucheza kwao soka la kulipwa kumekuwa na manufaa.
Mabeki wa DR Congo waliokuwa chini ya kiungo mkabaji wa Newcastle United, Chancel Mbemba walikuwa na kazi ngumu kudhibiti kasi ya Samatta na Msuva.
“Wachezaji ninaowajua na kuwafuatilia ni Samatta, Msuva na Thomas Ulimwengu. Ninawafahamu hao ndio nyota na tegemeo Tanzania,” alisema kocha wa DR Congo Florent Ibenge.
Banda alikuwa kiongozi bora wa safu ya ulinzi akishirikiana vyema na Kelvin Yondani, Shomari Kapombe na Gadiel Michael waliomdhibiti mshambuliaji mahiri wa Everton, Yannick Bolasie.
Mchango wa kina Samatta unaweza kuzaa matunda endapo Tanzania itakuwa na idadi kubwa ya nyota wanaocheza nje.
Baadhi ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa, lakini Taifa Stars imewafungia vioo ni Michael Lema wa Sturm Graz ya Austria, Orgeness Mollel (Famalicao-Ureno), Emily Mgeta (Vfb Eppingen- Ujerumani) na Hussein Sembi anayetarajiwa kujiunga na klabu ya Victoria Guimares ya Ureno.
Samatta, Banda watoa kauli
Akizungumza Dar es Salaam, Samatta alidokeza Tanzania inaweza kupata mafanikio endapo itakuwa na idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa.
“Taifa Stars itakuwa bora zaidi endapo tutakuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka ya kulipwa, natoa wito kwa wenzangu kufungua milango,” alisema Samatta.
Kwa upande wake Banda alisema kiwango cha mchezaji wa kulipwa ni kikubwa anapocheza michezo ya ushindani na ametoa wito kwa Simba na Yanga kuweka mfumo mzuri wa kuwatafutia wachezaji timu za nje.
“Kinachotusumbua ni woga wa kujaribu, nilikwenda Botswana kufanya majaribio Township Rollers, lakini kutokana na uthubutu wangu nilipata nafasi ya kujiunga na BDF XI,” alisema Rashid Mandawa.
Kauli za nyota hao ziliungwa mkono na Needkens Kebano wa Fulham ya England, alisema wachezaji wa Tanzania wanatakiwa kuondoka mapema kwenda kusaka timu nchi ya nje.
Mkwasa, Mogella wafunguka
Mshambuliaji nyota wa zamani wa timu za Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella alisema wachezaji wa Tanzania hawako tayari kucheza soka la kimataifa. “Tatizo lililopo ni kwamba maisha ya wachezaji wengi wanaona kucheza Simba na Yanga ndiyo wamemaliza na hakuna sababu ya kupiga hatua mbele,” alisema Mogella.
Pia kiungo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Charles Mkwasa alisema endapo idadi wachezaji wengi wa Tanzania wanaocheza nje wakitumika vyema itakuwa chachu kwa wengine kupiga hatua.
“Tuna safari ndefu kwenye soka, moja ya vitu ambavyo vinaweza kuisaidia timu ya Taifa ni kuwa na wachezaji wengi wanaocheza nje,” alisema Mkwasa.
Mchezaji mwingine wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayai alisema wachezaji wa Tanzania wanatakiwa kutumia vyema mashindano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu kujiweka sokoni.

No comments:

Post a Comment