Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara inaingia raundi ya 24 kuna timu zimeingia kwenye msitari hatari wa kushuka daraja.
Ligi tayari imeshagawanyika makundi matatu. Simba na Yanga zenyewe zimejipambanua kuwa ndiyo zinazowania ubingwa kwa udi na uvumba.
Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 54, huku Yanga ikiwa na pointi 52.
Kundi la pili linaongozwa na Azam FC yenye pointi 41 na Kagera Sugar zenye pointi 39. Hili ni kundi ambalo kimahesabu linaonekana kama linaweza kutwaa ubingwa, lakini kiuhalisia ni kwamba pointi walizonazo zinawawezesha zaidi kubaki Ligi Kuu na kuwa salama, kuliko kutwaa ubingwa.
Kundi la mwisho ni lile ambalo liko kwenye hatari ya kuteremka daraja. Ni kundi ambalo linabidi lichange karata zake vizuri kwenye mechi sita hadi saba ambazo baadhi ya timu zimebakisha, vinginevyo safari ya kurejea Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara msimu ujao itawakumba.
Zipo nyingi, lakini hizi ndizo zipo kwenye hatari zaidi ya kushuka daraja kama zisipojiangalia na kuwa makini kwenye mechi zao zilizosalia.
- JKT Ruvu
Kama ni kubeti, basi hii ni timu ambayo unaweza kuweka mzigo wako na kuitaja kuwa ni moja kati zile tatu ambazo zitashuka daraja.
Ingawa inawezekana ikabadilika, lakini bado haionyeshi kama ni timu imara ambayo inaweza kusimama na kushinda mechi zote zilizobaki.
Inashikilia mkia, ikiwa kwenye nafasi ya 16, kwa pointi zake 20 tu. Katika ya mechi 24 ilizocheza, imeshinda tatu tu, ikitoka sare mechi 11 na kufungwa michezo tisa.
JKT Ruvu ndiyo timu iliyofunga magoli machache zaidi kwenye Ligi Kuu, ikiwa imeweka wavuni magoli 10 tu, ikifungwa magoli 20.
Ina kazi kubwa mno ya kufanya ili kuukimbia mstari wa hatari ya kushuka daraja ikizingatiwa tangu ipande daraja ligi kuu miaka zaidi ya 15 iliyopita haijawaji kushuka daraja, msimu huu kazi wanayo kuepuka fedheha hiyo.
- Majimaji
Isipojiangalia itakwenda na maji. Inakamata nafasi ya 15, ya mwisho kutoka chini, ikiwa na pointi 22 tu.
Haikuanza vizuri msimu huu na kuweka rekodi ya kupoteza mechi mfululizo. Ujio wa Kalimangonga Ongalla ulionekana kuirudisha kwenye ‘reli’, lakini kwa siku za karibuni ugonjwa wake unaonekana kurudia.
Imeshinda mechi sita kati ya 23 ilizocheza, nne ikitoka sare na michezo 13 ikipoteza.
3.Toto Africans
Ni timu yenye uzoefu wa kupanda na kurejea kwenye Ligi Kuu. Imeshawahi kufanya hivyo mara kwa mara.
Ilirejea kwenye ligi msimu uliopita. Ni timu ambayo maisha yake kwenye Ligi Kuu huwa ni kuwa kwenye hatari kushuka daraja. Kuna wakati inaponyeka kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Kama kawaida msimu huu ipo kwenye hatari hiyo ikiwa kwenye nafasi ya 14, ikiwa na pointi 22 kama ilivyo Majimaji, imefunga magoli 16 na kufungwa mabao 23 katika michezo 23 iliyocheza mpaka sasa
Toto inanufaika na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, kwani Majimaji imefungwa magoli zaidi ya timu hiyo.
Msuli unahitajika zaidi kuweza kuibakisha timu hiyo Ligi Kuu.
4. African Lyon
Kwa pointi 23 ilizonazo, bado haiko salama. Inakamata nafasi ya 13, ikiwa imecheza mechi 23, ikiwa imeshinda nne, sare 11 na kufungwa mechi nane.
African Lyon, timu iliyopanda msimu huu, siyo ngeni kwenye Ligi Kuu, kwani imekuwa ikipanda na kushuka.
Timu hii inaonekana kukamia zaidi mechi ambazo inacheza na timu kubwa kama Simba, Yanga na Azam, lakini inapocheza na timu kaliba yake, imekuwa haifanyi vizuri, ndiyo maana pointi ilizonazo na mechi ilizocheza ni sawa na pointi moja kila mechi.
- Ndanda
Moja ya timu iliyoleta chachu kubwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, Ndanda FC. Hata hivyo, msimu huu haiko kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Inakamata nafasi ya 12 kwa pointi 24 ilizonazo, ikiwa ni moja ya timu zilizo kwenye hatari zaidi ya kushuka daraja.
Nayo pia imeshinda mechi sita kati ya 24 ilizocheza ikiwa imetoa sare sita na kufungwa mechi 12. Isipokaza msuli, msimu ujao wakazi wa Mtwara, Ligi Kuu wataisikia kwenye bomba.
- Mbao
Ikiwa ni timu ngeni katika mikikimiki ya Ligi Kuu Tanzania ni miongoni mwa timu sita zilizo kwenye hatari ya kushuka daraja, ikiwa imecheza michezo 24 na kujikusanyia pointi 27.
Mbao timu iliyopanda Ligi Kuu kwa mgongo wa kufutwa matokeo ya Polisi Tabora na Geita Gold ni kama walikua hawakujipanga na ushindani wa Ligi Kuu, kwani matokeo yake kwenye msimamo siyo ya kuridhisha/
Imeshinda michezo saba, imetoka sare michezo sita na kufungwa michezo 11.
Kama inataka kubakia Ligi Kuu msimu ujao inapaswa kukaza msuli ili kuweza kujinusuru na hali ya kurudi Daraja la Kwanza msimu uajo.
No comments:
Post a Comment