Yanga inahitaji matokeo ya ushindi au sare ya angalau mabao mawili kuitoa Zanaco na kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa leo.
Ni kibarua kizito hasa ukizingatia jinsi Zanaco walivyoonekana kuwa imara kimwili na kiuchezaji katika pambano la ugenini dhidi ya Yanga.
Ni kwa maantiki hio Yanga watahitaji kuweka kikosi imara zaidi bila kujali ‘siasa za hapa na pale’ za fulani hatufai kwa sababu alitufungisha mechi fulani. Hisia ziwekwe kando, matokeo yatafutwe. Mengine baadaye.
Zifuatazo ni sababu za kocha George Lwandamina kumuamini Haruna Niyonzima ambaye hajaichezea Yanga toka mechi ya watani wa jadi, Simba iliyopigwa wiki tatu zilizopita.
Anaweza kukaa na mpira
Moja ya mbinu kubwa ya Niyonzima ni uwezo kukaa na mpira bila woga mpaka wenzake wafunguke au ampite adui. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Yanga ina kiungo mmoja tu mwenye uwezo wa kuficha mpira miguuni bila kujali nani anamkaba au kivuli cha adui.
Wapo wanaodai anakaa na mpira sana kiasi cha kukwamisha falsafa ya ‘Daima Mbele’ bila kujua kuwa kuna mechi ngumu zinazomhitaji fundi mwenye uwezo wa kukaa na mpira ili kufungua njia kwa wenzake.
Anaweza kucheza na mwili
Niyonzima hakubarikiwa nguvu nyingi wala mwili mkubwa lakini ni mwepesi wa kunyambulika na kuwadanganya wanaomkaba kwa kugeuka haraka hivyo kuweza kupiga chenga hatari na kupunguza maadui dimbani.
Ni ngumu kupokonywa mpira kirahisi tu bila kufanyiwa faulo.
Anapiga pasi sahihi
Pamoja na kutajwa kuwa na mbwembwe nyingi zisizo na tija uwanjani, Niyonzima ana uwezo mzuri wa kupiga pasi za uhakika tofauti na viungo wengine wa Yanga ukimuondoa Thaban Kamusoko.
Pia ana uwezo wa kupiga pasi mchanganyiko kulingana na eneo na wakati. Anapiga pasi fupi na pasi ndefu bila shida.
‘First touch nzuri’
Mchezaji mzuri hutambulishwa na jinsi anavyougusa mpira kwa mara ya kwanza. Niyonzima ana uwezo mzuri wa kuupokea mpira na kuuamuru utulie kwenye miguu yake bila kuhangaika kuugusa mara kibao.
Kwa uchezaji wa nguvu wa Zanaco unahitaji mchezaji anayeweza kumiliki mpira kwa mguso mmoja na kufanya maamuzi ya haraka haraka.
Anafunguka haraka
Analaumiwa kupenda kucheza na jukwaa lakini ukichunguza utagundua hufanya hivyo kwenye mechi dhidi ya timu ndogo. Ni nadra kufanya hivo kwenye mechi kubwa.
Akicheza na mtu anayejua kama Kamusoko, Niyonzima ana uwezo mkubwa kufunguka kwa haraka haraka kuchezesha timu kwenda mbele.
Hata kabla ya kupokea mpira mara nyingi anajua amkwepe vipi mkabaji na autoe vipi mpira. Inategemeana tu na aina ya mechi, wachezaji walio pembeni yake.
No comments:
Post a Comment