Kila inapopangwa dhidi ya timu kutoka Misri, Algeria, Morocco, Tunisia, Morocco hata Sudan tu kwa Yanga inakuwa tabu tupu.
Afadhali mwaka juzi iliambulia ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya AL Ahly kabla ya kutolewa kwa mikwaju ya penalty nchini Misri.
Ndio maana watani wa jadi, Simba, wakisikia ratiba tu kwamba Yanga imepangwa dhidi ya timu kutoka Uarabuni, basi wanaanza kuwatania kuwa hapo ndiy mwisho wa safari yao. Na kweli inakuwa hivyo.
Waswahili husema kila mtu na mbabe wake, pia na mnyonge wake. Timu kutoka Comoro nazo zimekuwa na rekodi mbaya ya kutolewa kwa idadi kubwa ya mabao kila zinapopangwa dhidi ya Yanga kwenye michuano ya kimataifa.
Ingawa kwenye soka lolote linaweza kutokea , lakini rekodi zinaibeba Yanga na kuwa tayari wengi walishaona ni kama imeshavuka hata kabla ya kuisamabaratisha Ngaya de Mbe kwa mabao 5-1 hio jana katika mchezo wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Comoro.
Matokeo ya jana yalikuwa ni muendelezo wa historia ya kutofurukuta kwa timu za Comoro mbele ya Yanga. Timu za huko zinaiona Yanga nuksi kama Yanga yenyewe inavyoziona timu za waarabu.
Kabla ya kipigo cha jana, mara tatu timu za Comoro zimekuwa zikiambulia vichapo vitakatifu.
Zifuatazo ni mechi ambazo Yanga imecheza dhidi ya timu za Comoro.
Yanga 5-1 AJSM ( 2007)
Hii ilikuwa ni mechi ya kwanza Yanga kukutana na timu kutoka nchini Comoro. Ilichezwa nchini Comoro mwishoni mwa Januari dhidi ya AJSM na kuisasambua kwa mabao 5-1 katika Ligi ya Mabingwa.
Yanga ilifuzu bila kucheza mechi ya marudiano kufuatia AJSM kudai Comoro kulikuwa hakuna uwanja ambao unakidhi vigezo vya CAF.
Yanga 14-1 Etoile d’or Mirontsy ( 2009)
Ilikuwa ni mechi ya awali ya Ligi ya Mabingw a mwishoni mwa Januari 2009, Yanga ilicheza dhidi ya Etoile d’Or Mirontsy kutoka Comoro na kushinda kwa mabao 8-1.
Kama vile haitoshi, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 6-0 katika mchezo wa marudiano ugenini na kufanikiwa kusonga mbele kwa ushindi wa jumlaya mabao 14-1.
Yanga 12-2 Komorozine de Domoni ( 2014 )
Yanga iliendeleza ubabe kwa timu za Comoro mwaka 2014 ilipoishusha kipigo kizito kizito cha jumla ya mabao 12-2 timu ya Komorozine.
Awali mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa ilichezwa jijini Dar na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 7-0 huku Mrisho Ngassa akifunga ‘hat-trick’.
Kwenye mechi ya marudiano iliyochezwa nchini Comoro, Yanga iliendeleza kipigo kwa kuibuka na ushindi wa mabao 5-2, Ngassa akifunga mabao matatu tena.
No comments:
Post a Comment