Kaseja anazeeka na utamu wake - ALEX MWENDATZ

Breaking

Friday, February 24, 2017

Kaseja anazeeka na utamu wake

Ilikuwa kidogo asajiliwe na klabu ya Simba kwenye kipindi cha dirisha dogo la usajili msimu huu.
Hata hivyo kulikuwa na kupingana baina ya baadhi ya viongozi wa Simba, wengine wakitaka asajiliwa na wengine wakidai kuwa amezeeka.
Anayezungumziwa hapa ni golikipa mkongwe nchini Tanzania na Afrika Mashariki, Juma Kaseja.
Kitendo cha kukaa nusu msimu bila ya kuwa na timu yoyote, akiwa kocha wa makipa wa Serengeti Boys, pamoja na kucheza soka la ufukweni, lilimfanya kuonekana kuwa tayari uwezo na umri kwa pamoja vimemtupa mkono.
Kinyume chake, amechaguliwa na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kuwa mchezaji bora wa mwezi Januari kwa msimu huu wa ligi, 2016/17.
Kaseja amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi kutokana na kufanya vizuri akiwa na timu yake mpya ya Kagera Sugar.
Kocha Mecky Mexime aliamua kumuamini kipa huyo, mara baada ya uongozi wa klabu hiyo kumsimamisha kipa Hussein Shariff ‘Casillas’ aliyesimamishwa kwa muda usiojulikana kutokana na madai ya kuihujumu timu hiyo, ilipopokea kipigo cha mabao 6-2 kutoka kwa Yanga, Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Alikuwa akiwania uchezaji bora na wachezaji wengine wawili ambao ni Mbaraka Yusuph, straika ambaye pia anaichezea Kagera Sugar na Jamal Mtengeta wa Toto African.
Kutokana na kuwabwaga wachezaji wenzake hao, Kaseja atazawadiwa kitita cha Sh.Milioni moja kutoka kwa wadhamini wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Image result for juma kaseja
Kilichompa uchezaji bora wa mwezi ni takwimu zinazoonyesha kuwa alifungwa goli moja tu mweza Januari, kati ya mechi tatu alizocheza na kuiacha timu yake ikifungwa magoli sita.
Uwezo unaoonyeshwa na kipa huyo mkongwe, inaweza kuwa ni ishara kuwa bado ana uwezo wa hali ya juu kuidakia timu yoyote ile kwenye Ligi Kuu, zikiwemo zile kubwa za Simba, Yanga na Azam.
Lakini pia ni kengele ya hatari kwa makipa wengine vijana wanaochezea Ligi Kuu, kuwa uwezo walionao, bado haujaweza kumfikia kipa huyo pamoja na ukongwe wake alionao.
Kama akiendelea hivi, wala haitoshangaza kusikia akigombewa na klabu kubwa, baada ya Ligi Kuu kumalizika.
Kaseja ambaye ameshazichezea klabu kubwa za Simba na Yanga, timu yake ya mwisho ilikuwa ni Mbeya City msimu wa 2015/16, alipoichezea kwa mkataba wa miezi sita na baada ya hapo akawa nje ya soka kwa muda mrefu.
Historia yake ya soka inaonyesha kuwa alijiunga na Moro United mwaka 2000 akitokea Shule ya Sekundari Makongo.
Aliichezea kwa miaka miwili na kujiunga na klabu ya Simba aliyoichezea kwa muda mrefu kuliko timu nyingine yoyote, kwa mafanikio makubwa.
Moja ya mafanikio yasiyosahaulika ni kuwa mmoja wa wachezaji waliochangia Simba kuivua ubingwa wa Afrika, Zamaleki kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2003 na kutinga hatua ya makundi.
Kaseja alipangua penalti mbili nchini Misri na kuifanya timu yake kusonga mbele, baada ya kila timu kushinda bao 1-0 nyumbani.
Alijiunga na klabu ya Yanga kwa vipindi viwili, msimu wa 2008/09, pia 2013/14.
Pamoja nafasi yake ya ukipa, amefunga magoli mawili kwenye karia yake ndefu ya soka.
Msimu wa 2008/09 alifunga goli la umbali mrefu, Yanga ilipocheza dhidi ya Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na kuifanya timu yake iondoke na ushindi wa mabao 2-1.
Lingine ni kwenye mechi ya watani wa jadi akiwa na timu ya Simba.


Alifunga goli kwa mkwaju wa penalti, dakika ya 67, Simba iliiangamiza Yanga mabao 5-0, Mei 6, 2012.

No comments:

Post a Comment