Haikushangaza sana. Ndemla kama ilivyo kwa Niyonzima amejaliwa uwezo wa kupiga pasi zenye macho jambo ambalo alilithibitisha katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kama ulitazama vizuri pambano la jana hautamshangaa sana shabiki aliyepagawa na utamu wa pasi kuuliza kama ni kweli Ndemla amefungiwa rula mguuni.
Kikosi cha Simba kilipotoka kuna walioulizia kukosekana kwa jina la Ndemla katika orodha ya wachezaji wanaoanza. Na kweli, Simba ilionekana kupwaya mno katikati kwa Yanga kutawala pambano na kulifikia lango la Simba kwa haraka.
Simba walishindwa kabisa kutulia na mpira kiasi cha James Kotei kulazimika kucheza chini sana kusaidi safu ya ulinzi.
Maamuzi ya kumtoa benchi la ufundi la Simba kumtoa Juma Liuzio na kumuingiza dimbani Ndemla yalibadilisha sura ya mchezo.
Tangu alipoingia dakika ya 26 aling’ara kwa kupiga pasi zilizosambaza mpira kwa ufasaha wa kunawirisha mboni za macho ya mashabiki hadi wa timu pinzani, Yanga.
Dakika mbili tu baada ya kuingia Ndemla, Simba walifanya shambulio la kwanza la maana na hatimaye Laudit Mavugo kukosa nfasi hio ya wazi kwa kushindwa kulenga kichwa chake kwenye lango la Deogratius Munishi aliyekuwa ameshakubali yaishe dakika ya 29.
Dakika ya 39 alipiga pasi nyingine sahihi iliyomfikia mlengwa, Mohamed Ibrahim aliyefanikiwa kufanya jaribio zuri langoni mwa Yanga.
Dakika moja kabla ya mapumziko, utamu wa miguu ya Ndemla uliishibisha mboni za mashabiki wa Simba kwa pasi nyingine ya kupenyeza kwa Mo’ Ibrahim aliyesababisha kutendewa madhambi kwenye ukingo wa eneo la hatari na Simba kupata mkwaju wa adabu ndogo.
Miguu ya Ndemla iliendelea kuongea kipindi cha pili. Dakika ya 49 aligongeana vizuri pasi na Ibrahim Hajib kumtengenezea nafasi Laudit Mavugo ambaye hata hivyo alikuwa amejenga kibanda eneo la Yanga.
Dakika ya 51, alionesha jicho zuri la pasi ndefu kwa mpira wake kutua katika miguu ya Mavugo akiwa eneo zuri la pembeni na kumlazimu Vincent Andrew kumfanyia madhambi.
Pasi hio ya Ndemla ilizaa pigo huru na kikubwa zaidi ilisababisha Andrew kuoneshwa kadi ya njano iliyomfanya acheze kwa woga zaidi wa kupewa kadi nyekundu na hivyo kumpa mwanya Mavugo kumsumbua.
Kama ulikuwa makini kuutazama mpira basi uliona bao la kusawazisha la Simba likianzia kwenye miguu ya Ndemla aliyegonga pasi sahihi kwa Yassin Mzamiru aliyemsambazia Shiza Kichuya pasi aliyetenda kwa krosi safi kwa Mavugo kusukuma nyavuni mpira kwa kichwa murua.
Kama vile haitoshi Ndemla alihusika katika bao la Kichuya lililomaliza ubishi. Ilikuwa dakika ya 80 pale Ndemla alivyofanikiwa kumtambuka beki wa Yanga upande wa kushoto pembeni na kupiga pasi kwa Jonas Mkude aliyempigia pasi mfungaji Kichuya.
Ndemla ana mapungufu yake hasa katika matumizi ya nguvu kutokana umbile lake lakini kwa pambano la jana alidhihirisha ni kwa nini Niyonzima alimchagua kuwa mchezaji anayemvutia zaidi nje ya Yanga.
No comments:
Post a Comment