Rufaa ya Wambura yagonga mwamba - ALEX MWENDATZ

Breaking

Wednesday, April 4, 2018

Rufaa ya Wambura yagonga mwamba


Rufaa ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) Michale Richard Wambura imegonga mwamba baada ya kamati ya rufaa ya maadili ya TFF kuipiga chini katika kikao kilichokaa Jumamosi Machi 31, 2018.

Taarifa zinasema kuwa Wambura aliyekata rufaa akidai kuwa utaratibu uliotumika kusikiliza shauri lake katikati ya mwezi uliopita ulikiukwa lakini kamati ya rufaa imetaja kuwa hakukuwa na ukiukwaji wowote kwani taarifa ilimfikia na alipata muda wa kujitetea.

"Baada ya kupitia vielelezo na ushahidi kutoka sekretarieti ya TFF na maelezo kutoka kwa Mrufani kamati ya maadili ya rufaa ya TFF imefikia maamuzi yafuatayo," ilianza kwa kusema taarifa hiyo. 

Baada ya mahojiano 

"Baada ya mahojiano na mabishano ya pande zote mbili, kamati imeridhia kuwa mrufani Michael Wambura alipewa nafasi ya kusikilizwa japo hakutokea, mwito wa alipelekewa nyumbani kwake Machi 13 saa 12 jioni kufika mbele ya kamati Machi 14, 2018," imesema. 

Kamati hiyo ya rufaa imesema kuwa Pamoja na wakili wake kutaka apewe muda zaidi wa kuwasilisha utetezi, ombi ambalo kamati ilikataa, hivyo kamati ilikuwa na haki ya kusikiliza shauri la upande mmoja.

"Baada ya kutafakari kwa kina, tumeamua kuitupilia mbali rufaa ya ndugu Michael Wambura, hivyo uamuzi wa kamati ya maadili unabaki halali," imesema taarifa hiyo. 

Makosa yake 

Ikumbukwe kuwa Michael Richard Wambura ambaye ni makamu wa Rais TFF alifungiwa maisha kutojihusisha na soka kwa makosa matatu ya kutumia vibaya Ofisi ya TFF.

Tayari TFF chini ya kamati ya utendaji imeshamteua Athuman Nyamlani kuwa Kaimu Makamu Rais hadi pale uchaguzi wa kumpata Makamu mpya utakapofanyika. 

No comments:

Post a Comment