Sterling atoa neno Kombe la Dunia - ALEX MWENDATZ

Breaking

Wednesday, March 28, 2018

Sterling atoa neno Kombe la Dunia

  


London, England.Mshambuliaji wa England Raheem Sterling, amesema timu hiyo ina nafasi ya kucheza kwa kiwango bora katika fainali za Kombe la Dunia endapo wataungwa mkono na mashabiki.
Sterling alisema ana amini England inaundwa na wachezaji wenye ubora, lakini wanatakiwa kuungwa mkono na mashabiki wa nchi hiyo.
Fainali za Kombe la Dunia zimepangwa kuanza Juni 14, Russia na England ni miongoni mwa nchi zinazopewa nafasi ya kung’ara.
Mchezaji huyo wa Manchester City alisema wachezaji wanatakiwa kupata upendo ili kuwapa morali ya kucheza kwa kiwango bora fainali hizo.
England inatarajiwa kucheza mechi mbili ngumu, baada ya kuilaza Uholanzi bao 1-0 kabla ya jana kupepetana na Italia.
“Napenda kuona tukiungwa mkono, itakuwa faraja kuona kila mmoja akiwa nyuma yetu,” alisema Sterling.
Sterling mwenye miaka 23, amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu akiwa na rekodi ya kucheza mechi 36 za kimataifa.
“Kama unataka nchi yako kupata mafanikio ni vyema ukawaunga mkono vijana wapate moyo wa kucheza kwa kujiamini. Onyesha upendo, kila mmoja anatakiwa kuwa nyuma ya timu,” aliongeza kiungo huyo wa pembeni.
Alipoulizwa kama baadhi ya mashabiki wamekuwa wakiwavunja moyo, Sterling alikiri baadhi ya mashabiki wamekuwa wakitoa lugha kali dhidi yao timu inapocheza chini ya kiwango.
Pia mchezaji huyo amesifu kazi nzuri ya kocha wa Man City, Pep Guardiola kwa kumjengea uwezo wa kucheza soka kwa kiwango bora msimu huu.

No comments:

Post a Comment